This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-6/

Kuanzisha mfumo wa walimu wa muda unaosaidia mfumo wa Ufuatiliaji Sambamba katika elimu mjumuisho, Kambodia

Sandrine Bouille

Matumizi ya walimu wa muda ni dhana mpya nchini Kambodia. Jimbo la Battambang na wilaya ya Thmor Kol yanaongoza katika utekelezaji wake. Ministry of Education, Youth and Sport (MOEYS) Wizara ya Elimu, Vijana na Michezo iliiomba Jumuia ya Handicap International kuanzisha na kusaidia, kitaalamu na kifedha, utekelezaji wa mradi wa majaribio wa mfumo wa walimu wa muda katika shule 15 za kawaida za msingi kutoka kanda za Otaki na Chrey. Hapa, Sandrine anaelezea mbinu iliyotumika ya Ufatiliaji sambamba.

Kuanzisha mfumo wa walimu wa muda
Mfumo huu ulianza mwaka 2010 na kuajiri walimu wanne wa muda ambao husafiri kati ya shule za kawaida katika jamii kutoa ushauri, vifaa, na msaada kwa watoto wenye ulemavu, walimu wao, na wazazi wao. Wanaunga mkono dhana ya elimu mjumuisho na kuitangaza kwa wakurugenzi wa shule na walimu wa shule za kawaida.

Majukumu yao makuu ni:

  • kuwasaidia watoto wenye ulemavu madarasani na nyumbani
  • kutoa ushauri na msaada kwa walimu
  • kutambua, kuwafanyia uchunguzi, na kuwapa rufaa watoto wenye ulemavu
  • kutoa mafunzo kwa walimu na jamii pamoja na kufanya shughuli mbali mbali za uhamasishaji katika jamii.
  • kufanya kazi na watoto wa umri tofauti na wenye changamoto mbalimbali.

Kupanua wigo wa walimu wa muda
Ufafanuzi wa kazi za walimu wa muda unasisitiza msaada kwa ajili ya mahitaji binafsi ya watoto wenye ulemavu. Hata hivyo, ni machache kati ya majukumu haya yanayoshughulikia vikwazo vinavyowakabili watoto wenye ulemavu ndani ya shule au kukuza dhana ya elimu mjumuisho.

Mara moja ilikuwa ni dhahiri kwamba walimu wa muda katika mfumo huu hawawezi kulenga watoto wenye ulemavu tu lakini lazima pia kuzingatia ubora wa elimu ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wote. Kulikuwa na haja hasa kwa walimu wa shule za kawaida kuelewa dhana ya elimu mjumuisho na kuendeleza mjumuisho katika ufundishaji.

Mbinu ya ufuatiliaji sambamba na umuhimu wake.
Jumuia ya Handicap International inaelezea mfumo wa ufuatiliaji sambamba katika elimu mjumuisho kama ifuatavyo:

“Ujumuishaji wa watoto wenye ulemavu katika elimu ya kawaida unahitaji kukuza na kutumia njia za mjumuisho katika ngazi zote, badala ya kuzingatia ulemavu wa mtoto tu … [hii ni] mbinu ya ufuatiliaji sambamba, ambapo mahitaji binafsi ya watoto wenye ulemavu yanapatiwa ufumbuzi sambamba na kushughulikia vikwazo vya kijamii, kimazingira, kiuchumi na kisiasa katika elimu”.1

Kushughulikia ulemavu wa mtoto tu kunatoa hisia kuwa mtoto ndio tatizo kwa sababu yeye anahitaji huduma, vifaa au msaada maalum. Mbinu ya Ufuatiliaji sambamba inapunguza kushughulikia mtu binafsi bila kuakisi chochote katika marekebisho muhimu yanayohitajika katika mfumo wa elimu. Kinyume chake, kufanya kazi katika ngazi ya mfumo wa elimu pekee kunaweza kuchangia kupuuza mahitaji binafsi ya kila mtoto. Kuzifanyia kazi ngazi zote hizi mbili ni muhimu kwa kujenga mazingira bora kwa watoto wenye ulemavu na ngazi zote mbili kwa wakati mmoja ni muhimu sana katika kuwatengenezea mazingira mazuri watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu kujifunza na kufanikiwa katika shule na kuhakikisha kuwa watoto wanapewa haki na fursa sawa katika elimu.2

Ufuatiliaji Sambamba katika mfumo wa walimu wa muda
Ili kuepuka kuwabebesha mzigo mkubwa walimu hao wa muda, na ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mfumo wa elimu, mradi huu ulihamasisha ushiriki wa wazazi, na wengine katika jamii (maafisa wa afya wa vijijini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu). Ifuatayo ni baadhi ya mifano halisi ya mbinu ya ufuatiliaji sambamba:

Kushughulikia mahitaji binafsi ya watoto wenye ulemavu
Kwa miaka mitatu, mfumo huu umekuwa ukishughulika na Ratanak – kijana wa kiume (sasa miaka 15) ambae yuko darasa la 43, asiyeoona – kumpatia vifaa kama vile mashine ya Breili na abakasi. Wakati wa masomo mwalimu wa muda humsaidia moja kwa moja Ratanak darasani ili aweze kufuata masomo kama yanavyoendelea katika shule ya kawaida na pia humsaidia kuweza kupata stadi maalum. Hakuna masomo ya mtu mmoja mmoja au mazoezi yanayotayarishwa kwa Ratanak peke yake lakini njia za ufundishaji hubadilishwa kwa mujibu wa hali yake ili aweze kushiriki. Idadi ya mara zinazohitajika kumsaidia hubadilika kutegemea na maendeleo yake. Mwanzoni, msaada ulikuwa ni kila siku, lakini leo ni kila wiki.

Mwalimu huyu wa muda alimsaidia mwalimu wa Ratanak kwa kumpa ushauri na mbinu, kama vile kusoma kwa sauti na kusoma kilichoandikwa katika ubao,kurudia mara kwa mara, na kumpa Ratanak muda zaidi wa kuandika katika Braille au kutumia Abakasi. Msaada wa rika kwa rika pia ulianzishwa, ili mwanafunzi mwingine aweze kumsaidia Ratanak wakati wa masomo pindi akihitaji maelezo ya ziada au maelekezo wakati mwalimu huyo hayupo.

Walimu hawa pia wana jukumu la kutambua mahitaji maalum ya watoto wenye ulemavu kuhusu huduma za afya na / au hatua za kushughulikia hali zao.

Kushughulikia vipingamizi vilivyomo ndani ya shule
Sopheap ni kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 16 mwenye ugonjwa wa Down’s Syndrome (Sura mfanano). Alifukuzwa shule kutokana na maswala ya tabia; alikuwa akipambana na wale waliokuwa wakimchokoza na kumzomea. Vikao vya uelimishaji kwa wanafunzi kwa kutumia vitabu vya hadithi za kuchekesha, vikatuni, hadithi na mabango vilisaidia kupeleka ujumbe kuhusu uvumilivu na kuthamini tofauti na utofauti. Jambo hili lilikuza mshikamano miongoni mwa wanafunzi. Sopheap sasa yupo tena shuleni. Amekuza stadi na tabia zake kwa kiwango kikubwa kwa vile marafiki zake wamekuwa ni marafiki wazuri zaidi na wenye mtazamo chanya zaidi kwake. Walimu wa muda hutayarisha vikao vya kila mwezi vinavyojadili kuhusu kukuza mawasiliano na watoto, usimamizi wa tabia, usimamizi wa darasa na kujenga uwezo wa kujiamini kwa watoto. Vikao hivi vina lengo la kuinua ubora wa elimu. Baadhi ya walimu wana shauku ya kutaka kuzifanyia kazi mbinu mpya na hatua kwa hatua huwashawishi walimu wengine. Mwalimu wa Sopheap hususan, alifurahia mafunzo juu ya kanuni za darasa, kwa sababu kanuni zilizo wazi – zilizofafanuliwa na kukubaliwa kwa pamoja kati ya uongozi wa shule na wanafunzi – humwezesha mwalimu kupata muda wa kushughulikia ufundishaji na kuwasaidia wanafunzi zaidi kuliko kushughulikia maswala ya nidhamu. Kila mwaka, vikao kadhaa vya utengenezaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia hupangwa katika kila shule. Vifaa vinavoundwa ni muhimu kwa ajili ya kusaidia mitindo mbalimbali ya kujifunza na kufundishia kwa njia ya kucheza,ambayo inakuza ubora wa ufundishaji. Nyenzo zilizotengenezwa wakati wa vikao hivi huwanufaisha wanafunzi wote, na mabadiliko hufanywa kukidhi mahitaji maalum ya watoto wenye ulemavu. Kwa mfano, mwalimu wa elimu ya kawaida wa Ratanak alitengeneza kadi yenye maneno yaliyoandikwa kwa lugha ya Kikhmeri na katika maandishi ya Breili. Kwa njia hii, Ratanak anaweza kushiriki katika michezo na wanafunzi wenziwe.

Athari za mfumo wa Ufuatiliaji Sambamba
Mwanzoni mwa mradi, walimu wa muda walikuwa mara nyingi wakionekana kama ni walimu maalum wenye dhamana ya kufundisha watoto wenye ulemavu, hivyo walimu wa elimu ya kawaida waliwategemea sana kusaidia watoto wenye ulemavu. Matumizi ya mbinu ya Ufuatiliaji Sambamba yaliwawezeshwa wafanyakazi wa shule kuwafahamu vizuri zaidi walimu hawa wa muda kuwa ni watetezi na wafuasi wa elimu mjumuisho, mbinu ambayo haiishii katika utoaji wa elimu maalum katika mazingira ya shule za kawaida tu. Walimu wa elimu ya kawaida sasa wanafahamu kuwa walimu hawa wa muda ni waelimishaji waliohitimu ambao wanaweza kutoa ushauri juu ya ufundishaji kwa ujumla pamoja na kuwa ni wataalamu katika maswala yanayohusiana na ulemavu.

Hatimaye, mbinu ya Ufuatiliaji sambamba imetoa ufahamu mzuri juu ya maana ya elimu mjumuisho; si elimu inayolenga watoto wenye ulemavu tu na kulenga katika kushughulikia matatizo yao maalum ya ulemavu, lakini ni elimu ambayo ina lengo la kutoa elimu inayofaa na yenye ubora kwa watoto wote kujifunza pamoja.

Mradi uliopo sasa utamaliza muda wake Disemba 2013

Handicap International,
Programu ya Kanda ya Kambodia & Thailand
S.L.P 586 /P.O. Box 586, Khan Chamkar Mon, Phnom Penh, Ufalme wa Kambodia
www.handicap-international.org

Kwa habari zaidi zinazohusu mtazamo wa Handicap International katika Elimu Mjumuisho, wasiliana na: Gilles Ceralli, Mshauri wa Kiufundi wa Elimu Mjumuisho, GCERALLI@handicap-international.lu

1 Handicap international, Policy brief, Inclusive Education, September 2012, p.4
2 Kama ilivyoelezwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Watu wenye Ulemavu, Kifungu cha 24.
3 Nchini Kambodia, elimu ya msingi ni kutoka darasa la I hadi la VI. Watoto huanza shule wakiwa na umri wa miaka 6.