This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-5/

Kutafiti Jawabu Zangu Mwenyewe:Mahojiano na Mwalimu wa Mjumuisho, Malaysia

Rosnah Sahilan amekuwa akifundisha kwa miaka sita sasa. Ana Shahada ya kwanza ya Biotechnology na Shahada ya Ualimu. Hapa anaelezea raghba yake ya kuwasaidia watoto wote darasani kwake na vipi amezifanyia majaribio mbinu alizobuni mwenyewe kuhusiana na changamoto za mjumuisho.

Una fikra gani kuhusu mjumuisho kwa ujumla?
Nadhani kwamba kila mtoto ana kipaji; ni jukumu letu sisi walimu kugundua vile walivyonavyo watoto. Mambo ambayo si mazuri yako katika mazingira ya shule. Kadiri tunavyojitahidi kuwaelewa watoto, haitakuwa tatizo kubwa. Kinachohitajika ni kufanya utafiti, ili tuelewe vizuri zaidi mahitaji yao katika shule na kile wanachohitaji kutoka kwetu sisi kama walimu.

Kwa nini unapendezwa na utafiti kuwa sehemu ya kazi yako ya kufundisha?
Nchini Malaysia bado baadhi ya walimu wana mtazamo hasi kuhusu watoto wenye ulemavu. Hatujazoea sana hali kama ya autism au ADD (Attention Deficit Disorder) (Upungufu wa Umakini). Walimu hawajui chochote kuhusu hali hizo. Nadhani walimu wote wanahitaji kufunzwa namna ya kushughulikia hali ya aina hii. Ndio maana mimi nina haja ya kufanya utafiti ili unisaidie mwenyewe. Mimi ningependa sana kuwajumuisha watoto wenye ADD na autism. Jambo hili linanipa changamoto katika mbinu zangu za kawaida. Ninawaza: “Ninawezaje kuwajumuisha pamoja na marafiki zao katika kufundisha na kujifunza? Jinsi gani naweza kuwasaidia katika darasa?”. Daima nimekuwa nikijaribu kufikiri ufumbuzi kwa kufanya vitendo vingi na mbali mbali, kutaka kujua vitendo vizuri na vile ambavyo si vizuri. Kwa njia ya kujaribu, nimepata ufumbuzi mzuri kwa watoto, unaosadifu tabia na sifa zao. Kila mtoto ni tofauti, hakuna watoto wawili walio sawa hata kama wana ulemavu wa aina moja.

Ni shughuli gani za utafiti umefanya?
Mimi ni mwalimu wa sayansi, ninapenda kufanya utafiti na kutafuta majibu. Najua kwamba baadhi ya aina za ulemavu zinahusiana na ubongo na kemikali, n.k, lakini si kosa la mwanafunzi au wazazi wao.

Mshauri wangu alinisaidia. [Rosnah amekuwa akishiriki katika mradi wa kupeleka washauri kwa walimu wa lugha ya Kiingereza ili kusaidia kuinua ubora wa ufundishaji lugha ya Kiingereza.] Nilimweleza kuhusu kupenda kwangu kuwajumuisha wanafunzi fulani na yeye alinipa msaada. Alinisaidia kutafuta vitabu na kuniunganisha na walimu wengine wenye uzoefu wa autism ambao wangeweza kunipa ushauri wa vitendo, ambao nimeutumia darasani. Nimetumia intaneti kupata mawazo, lakini hasa mimi huwa nina jaribu mbinu mbali mbali mimi mwenyewe. Nachunguza kama ni mbinu nzuri au la, kisha nafanya mabadiliko.

Umejifunza nini kwa njia ya utafiti? 
Nimeona kwamba watoto wenye ADD na autism wanataka kuwa kama wanafunzi wengine. Namna wanavyofikiri na kufanya mambo ni tofauti kidogo na wanafunzi wengine, lakini bado wanataka na wanahitaji mambo sawa. Sitaki kuwaweka kando, nataka niwajumuishe na wenzao. Inachukua muda. Watoto ambao ni wageni katika mazingira ya skuli wanaweza kuchukua muda wa ziada kuzoea utaratibu wa mambo katika shule.

Pia nimejifunza kwamba ni rahisi kukuza mtazamo chanya katika umri mdogo. Ni rahisi kwa wanafunzi darasani kumkubali mtoto mwenye autism, wanamheshimu na hawamfanyii uonevu – ingawa naweza kuhitaji kuwaelezea tangu awali kuhusu autism na kukataa kukubaliana na uonevu wowote. Inaweza kuchukua muda, lakini baada ya hapo watoto wanakuwa na mitazamo yao mipya ambayo ni chanya baadae katika maisha yao.

Kitu gani kimesaidia utafiti wako?
Kwa upande wangu, wazazi wameunga mkono watoto wao na wamewapa habari na kutoa ushirikiano kwa walimu. Hii ni faida niliyoipata, ingawa najua baadhi ya wazazi pengine hawazungumzi na walimu juu ya madai yao.

Rosnah anaweza kupatikana kupitia EENET.