This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-4/

Kufikiria Upya Mafunzo ya Ualimu, Bulgaria

Margarita Asparuhova

Mtazamo wetu wa ujumla
Mwaka 2007 tulianza kubuni na kuandaa mafunzo kwa walimu wa shule za kawaida kuhusu jinsi ya kuwasaidia na kuwafundisha watoto wenye mahitaji maalum ya kielimu katika mazingira ya shule za kawaida. Kwa wakati huo walimu wengi wa Kibulgeri walikuwa bado wana wasiwasi juu ya faida ya elimu mjumuisho na walikuwa hawana uhakika nini cha kufanya wanapokuwa na mtoto mwenye ulemavu katika madarasa yao.

Katika kazi yetu katika Centre of Inclusive Education – CIE (Kituo cha Elimu Mjumuisho) tumekuwa tukijaribu kutumia mbinu za ubunifu. Mafunzo yetu yanalenga kuwasilisha maarifa mapya na mbinu mpya juu ya mjumuisho zinazoendana na mahitaji na uhalisia wa shule. Kwa hiyo malengo yetu ni:

  • kufanya mitazamo ya walimu katika elimu mjumuisho kuwa chanya zaidi;
  • kuwasaidia walimu wa elimu ya kawaida, jinsi ya kufanya mazingira ya shule kuwa jumuishi kwa wanafunzi wao;
  • Kuwasidia walimu wa elimu ya kawaida kuanzisha na kuendeleza mbinu za kufanya kazi kwa mashirikiano na wazazi na wataalamu ambao wanawasaidia wanafunzi katika shule zao;
  • kuhamasisha walimu kutambua, kutumia na kupongeza uwezo walionao wanafunzi wao;
  • kuchangiana mawazo na walimu kuhusu mifano ya mambo mazuri ya kuigwa kutokana na uzoefu halisi walionao wakufunzi wetu;
  • kuwashirikisha walimu katika majadiliano ya mifano maalum, na vikundi vidogo vidogo katika warsha, hivyo kuwawezesha kutafakari zaidi juu ya mazoea yao na wakati huo huo kuwashajiisha kujiamini katika uzoefu wao wa kitaalamu na mbinu za kufundishia;
  • kuongeza uelewa na kuelekeza nguvu katika kile kinachoitwa ulemavu usioonekana, kama vile disleksia (kutoweza kusoma vizuri), disgrafia (kutoweza kuandika vizuri), dispraksia (dyspraxia), ADHD (Tatizo la Ukosefu wa Umakinifu) na autism.

Ingawa CIE hutoa mafunzo ya mada kwa ajili ya walimu wa elimu ya kawaida jinsi ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu ya kielimu katika mazingira ya shule za kawaida, shirika letu si shirika hasa la mafunzo. Timu yetu kwa sasa hushiriki katika miradi kadhaa inayohusiana na mjumuisho, ambayo inatupa fursa ya kuchukua mbinu muhimu zaidi kwa njia ya sisi kutoa mafunzo kwa walimu wa elimu ya kawaida na wadau wengine (wataalamu, walimu wasaidizi, wazazi). Uhusiano huu na hali halisi ya kazi ya mradi inatuwezesha kufanya mabadiliko sahihi katika mafunzo yetu, ili kuweza kukidhi mahitaji ya walengwa na hatimaye kufikia lengo letu la kuzifanya shule nyingi zaidi ziwe na mazingira ya kuvutia, walimu kujiamini zaidi, wazazi wenye ufahamu zaidi na bila shaka, watoto wenye furaha zaidi.

Miradi yetu 
Mradi wetu, ‘Shule Moja kwa Wote’,1 unalenga kurekebisha ili kuendana na mazingira na kutumia kote nchini Bulgaria, toleo la tatu la Vigezo vya Mjumuisho.2Mradi huu umeshabaini kuwa mitazamo ya walimu inaweza kubadilika kwa kiwango kikubwa kupitia uwezeshaji wenye uangalifu na kuheshimiana juu ya maadili, tafakuri binafsi, mazoea na malengo yao wenyewe. Hivyo, walimu wamekuwa na uwezo wa kutathmini mawazo na vitendo vyao wenyewe kwa makini na kuweza kubadilika kwa mujibu wa mahitaji ya wadau wengine (watoto, wazazi, na wenzao).

Mradi mwingine wa CIE, ‘Shule pia ni Haki Yangu’,3 unahusisha wadau kutoka shule mbili (za msingi\ sekondari) na nyingine mbili za chekechea ( kindergartens) katika mji mmoja wa Bulgaria. Mradi huu unataka kukusanya katika sehemu moja mitazamo ya walimu, wataalamu, wazazi, watoto na wawakilishi wa Mamlaka ya Elimu kuhusu fursa na changamoto kwa ajili ya kuendeleza elimu mjumuisho kwa watoto wenye mahitaji maalumu ya kielimu, wenye umri wa miaka 3 hadi 10. Mradi huu umetuwezesha sisi kutumia mbinu shirikishi zaidi kuliko mbinu za ‘kuhubiri’ katika mafunzo ya walimu, kama vile majadiliano ya vikundi, vikao vya ushiriki wa watoto kuwapasha habari watu wazima, na warsha za kujifunza kwa njia ya uzoefu ili kujenga uwezo.CIE pia ni mshirika ndani ya mradi wa Umoja wa Ulaya uitwao FIESTA4 Mradi huu umekuwa na nafasi kubwa katika kutengeneza vizuri ajenda yetu ya mafunzo ya ualimu. Kama sehemu ya mradi, mapitio ya rejea na ukusanyaji wa data katika maeneo ya utafiti ulifanyika katika nchi nane za Umoja wa Ulaya kuwajulisha ripoti ya utendaji katika mjumuisho, na kazi ya usimamiaji na ushirikiano katika kipindi cha mpito.5

Kubadilisha mwelekeo wa mafunzo
Katika kuiweka vizuri ajenda yetu ya mafunzo ya ualimu, tumekuwa tukibadilisha mwelekeo kutoka mwelekeo wa mada za uchunguzi hadi katika semina zenye lengo la kuwawezesha washiriki kuwa na uelewa mkubwa zaidi juu ya uwezo walionao watoto na pia ulemavu wao. Mwelekeo huo hutegemea zaidi juu ya kuangalia moja kwa moja katika mazingira yake mtoto kitamaduni na kijamii. Kwa mfano, miaka minne iliyopita neno ‘disleksia’ lilikuwa ni vigumu kujulikana na watendaji. Sasa linatumiwa kupita kiasi kwa kuelezea aina zote za matatizo ya kuweza kusoma,hali ambayo inaweza kubadilisha uhalisia na umakini katika kuona sababu nyengine zinazopelekea watoto kupata changamoto za kuweza kusoma (kama vile watoto kupata majeraha ya kihisia (kiwewe) au changamoto za kuweza kusikia au kuona; uwezo duni wa mwalimu katika kutumia mitindo au kasi ya ufundishaji, kwa mujibu wa hali za wanafunzi n.k).

Kwa sababu hiyo,’mbinu ya uchunguzi’ haiwasaidii sana walimu kuweza kuwasaidia wanafunzi kwa ufanisi. Hali kama vile disleksia, ADHD na autism zinajitokeza katika njia nyingi tofauti, na haiwezekani kutoa mafunzo kwa mwalimu jinsi ya kumfundisha mwanafunzi mwenye changamoto hizo kupitia mafunzo ya siku moja tu. Mbinu bora zaidi ni kutoa mafunzo kwa walimu kwa upana zaidi kuhusu utaratibu mzima wa hali ya kujifunza unavyokuwa (kumbukumbu, umakini, kazi za kumbukumbu, n.k); jinsi ya kutambua matatizo fulani pamoja nao, na mikakati gani inaweza kusaidia kuwa na hali nzuri ya kujifunza. Ni muhimu pia kwamba walimu wapewe mafunzo ya kuweza kujadili mambo haya kwa kujiamini wakiwa pamoja na wataalamu wa maswala ya watoto, wazazi wao, na bila shaka, watoto wenyewe.
Hata kama bado walimu wengi hadi sasa wanatarajia kupewa maelekezo ya kutatua changamoto ( badala ya wao wenyewe kuwa na uwezo huo), idadi kubwa ya walimu hao wameweza kufaidika kutokana na tafakuri binafsi na mbinu shirikishi, ambazo CIE ilitumia katika mafunzo yao. Ingawa mabadiliko hayo katika ajenda ya mafunzo ya walimu yanahitaji muda mwingi na juhudi kubwa, inawezekana na ni muhimu kufanyika. Aidha, ni hatua za kimantiki muhimu katika kuelekea kuwapokea watoto wenye mahitaji maalum ya kielimu katika shule za kawaida.

Kituo hiki cha Elimu Mjumuisho ni shirika la Kibulgeria lisilo la kiserikali, ambalo lengo lake kuu ni kukuza elimu mjumuisho kwa kila mtoto. Kituo hiki kinaendeleza kazi ya miaka kumi iliyoanzishwa na Shirika la Save the Children la Uingereza nchini Bulgaria na katika kanda hii. Kituo kinaamini kwamba kila mtoto lazima apewe nafasi ya kukubaliwa na kuthaminiwa, na kinafanya kazi kwa ajili ya mjumuisho wa kijamii na ubora wa elimu kwa watoto wote na kuwalinda wale wanaohitaji kulindwa. Timu ya Kituo hiki inafanya kazi pamoja na wazazi, walimu, mameneja, wataalamu, mamlaka za serikali za mitaa na dola, mashirika ya kibiashara, kitaifa na jumuia nyingine za kimataifa.

Margarita Asparuhova, Meneja wa Mradi,
Kituo cha Elimu Mjumuisho
Bulgaria, Sofia 1000, 60 Ekzarh Yosif Str, m.asparuhova@cie-bg.eu

Kujenga uhusiano kwa ajili ya Mjumuisho
A group of mainstream teachers, specialists and resource teachers is communicating to other participants an idea with gestures only. The aim of the activity is to emphasise empathy and attentiveness in education. A mainstream and a resource teacher are drawing together with one pencil. The aim of the activity is to provoke self-reflection on team working, leading and following a lead.
Kikundi cha walimu wa shule za kawaida, wataalamu walimu washauri kikiwasiliana na washiriki wengine kuhusu wazo fulani kwa kutumia alama tu. Lengo kubwa la zoezi hili ni kusisitiza upendo na umakini katika elimu. Mwalimu wa shule ya kawaida na mwalimu mshauri wakichora kwa pamoja kwa kutumia penseli moja. Lengo la zoezi hili ni kuanzisha tafakuri binafsi juu ufanyaji kazi kwa mashirikiano, kuongoza na kufuata katika kuongozwa.
Mwaka 2013, CIE ilitayarisha warsha ambayo ilikuwa ni sehemu ya mradi wa School is my Right too (Shule pia ni Haki yangu), iliyokusudia kuongezea nguvu mahusiano – kuaminiana na kushirikiana miongoni mwa walimu wa shule za kawaida, wataalamu na walimu washauri ambao huwasaidia watoto waliotambuliwa kuwa wana mahitaji maalum ya kielimu katika mazingira ya shule za kawaida.
“Maoni tuliyopata kutoka kwa washiriki yalijikita zaidi katika faida zilizotokana na kukutana na watu wengine na hivyo kupelekea kila mmoja kufahamu dhamana, matarajio na changamoto za wenzake, jambo ambalo kwa maneno yao wenyewe “litakuza mashirikiano yao baadae”Maria Tasheva, Mratibu wa mradi
Tutatoa Makala kubwa zaidi kuhusu athari ya warsha hii kwa mujibu wa maoni ya washiriki juu ya majukumu yao kila mmoja na kuhusu wanavyofanyakazi pamoja, katika EENET toleo la 2014 la “Kuwezesha Elimu”

 

Vigezo vya Mjumuisho Vimetajwa sehemu kadhaa katika jarida hili.

Nini maana yake?
Kwa urefu zaidi ni: ‘Vigezo vya Mjumuisho: Kuanzisha Ujifunzaji na Ushiriki katika elimu. Iliandikwa kwanza na Tony Booth na Mel Ainscow na kufanyiwa majaribio 1997/8. Vimepitiwa upya mara tatu, ya karibuni zaidi ni ya Tony Booth mwaka 2011, na vimechapishwa na Kituo cha Taaluma za Elimu Mjumuisho. Vigezo vya Mjumuisho ni kitini kinachoziwezesha shule kujifanyia tathmini binafsi na kujisahihisha kulingana na tathmini hiyo. Vinatoa mwongozo halisi ili jamii nzima ya shule iweze kufanya kazi ya kupitia upya mambo yote ya shule hiyo yahusuyo utamaduni, mitazamo, sera na matendo. Vinasaidia pia shule kutafakari juu ya maadili yao, kujifanyia tathmini na kuinua uwezo wa shule. Vinatoa mwongozo na ushauri utakaowezesha jamii nzima ya shule kushirikiana katika kupitia kanuni na sera na taratibu mbali mbali za shule kwa lengo la kuziimarisha ziwe bora zaidi. Vigezo hivi huzisaidia shule kutafakari juu ya maadili yao, kutekeleza tathmini binafsi kutoka katika mtazamo wa wadau mbalimbali; kuendeleza mambo mbali mbali yatakayosaidia shule kimaendeleo na kufanya kazi kwa kupunguza vikwazo vya kujifunza na ushiriki. Vigezo hivi vilitungwa nchini Uingereza, lakini vimekuwa vikitumiwa na kuleta mafanikio katika nchi nyingine kadhaa duniani.

Nakala zake zinapatikana wapi?
Unaweza kupata nakala za vigezo hivi katika toleo la 2000 bila ya malipo katika tovuti ya EENET http://bit.ly/1gFAcTZ
Toleo la 2011 linaweza kununuliwa kutoka CSIE: http://bit.ly/19xn0MJ

Wapi ninaweza kupata maelezo ya jinsi ya kuvitumia vigezo hivyo?
Katika tovuti ya EENET na majarida yake, kuna makala mbalimbali kuhusu vigezo hivi na jinsi vilivyofanyiwa marekebisho katika nchi mbalimbali. Kama umekuwa ukifanya kazi katika kutafsiri na kurekebisha vigezo hivyo, tungependa kupokea makala inayoeleza jinsi ulivyovitumia na matokeo yake yalivyokuwa.

1 One School for All (‘Shule Moja kwa Wote’) ni mradi unaofadhiliwa na European Social Fund ( Mfuko wa Jumuia ya Ulaya) kupitia Operational Program ‘Human Resources Development’ (Programu ya Utendaji ya ‘Maendeleo ya Rasilimali watu’).
Index for Inclusion (‘Vigezo vya Mjumuisho): Kukuza Ujifunzaji na Ushiriki katika Shule ‘, Booth, T., Ainscow, M., imepitiwa upya na Tony Booth, 2011, imechapishwa na Kituo cha Mafunzo ya Elimu Mjumuisho, Uingereza.
3 School is my right too (‘Shule pia ni Haki Yangu’) ni mradi unaofadhiliwa (kwa sehemu tu) na Jumuia ya Open Society Foundations.
4 Mradi wa Facilitating Inclusive Education and Supporting the Transition Agenda (FIESTA) (Uwezeshaji wa Elimu Mjumuisho na Kusaidia Ajenda ya Mpito) unafadhiliwa na European Commission (Kamisheni ya Ulaya)
5 Ripoti hii itapatikana katika mtandao kuanzia mwisho wa mwaka 2013: www.fiesta-project.eu