This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-3/

Kupitia upya mawazo ya msingi juu ya elimu mjumuisho India

Kanwal Singh na Ruchi Singh

Mara nyingi EENET imekuwa ikionesha kuwa kila mtu ana ufahamu wake na tafsiri yake kuhusu elimu mjumuisho. Hatua muhimu katika kuendeleza shule mjumuisho na mifumo ya elimu ni kwa watendaji na watunga sera kutafakari kwa kina juu ya imani zao na mawazo yao wenyewe. Katika makala hii, Kanwal na Ruchi wanatafakari kuhusu mvutano kati ya elimu maalum na elimu mjumuisho nchini India, na kuhusu mabadiliko ya mawazo yao wenyewe kuhusu elimu mjumuisho; mchakato ambao umesababisha mafanikio yao zaidi katika utekelezaji wa elimu mjumuisho.

Muongo mmoja uliopita, elimu mjumuisho nchini India ilikuwa ni mada mashuhuri katika majadiliano miongoni mwa walimu wa elimu maalum. Ilianza kama mtazamo maalum kwa kuwalenga watoto wenye ulemavu tu. Lengo lilikuwa kuwahamisha wanafunzi hao kutoka shule maalum na kujiunga na shule za kawaida na wakati huo huo kuwapatia watoto hao msaada na vifaa vya kutosha. Ilikuwa ni jambo la kusisimua- tulijifunza msamiati mpya na tulifurahia kuweza kuleta mabadiliko!

Katika akili zetu, hakukuwa na shaka kuhusu elimu mjumuisho. Hata hivyo, tulipata shaka kidogo wakati tukiwa katika matayarisho ya kuhama kutoka kwa nini hadi jinsi ya utekelezaji wa elimu mjumuisho. Kulikuwa na maswali kadhaa yaliyokuwa yakituumiza vichwa. Je, shule za kawaida zilikuwa ziko tayari? Zilikuwa haziwezi kufikiwa na wote. Hazikuwa na vifaa wala visaidizi vyovyote. Je, walimu walikuwa wametayarishwa? Vipi wangeweza kufundisha watoto wetu katika darasa lenye wanafunzi 50? Je, wanafunzi wataweza kuzoea katika mfumo unaojali zaidi mitihani? Ni nani wangechukua jukumu la tiba, mosomo ya mwanafunzi mmoja mmoja, na mahitaji ya kila siku? Je, watoto wengine hawatawachokoza na kuwakebehi watoto wetu? Mijadala moto moto ilikuwa ikiendelea miongoni mwa jamii ya elimu maalum. Waelimishaji wengi wa elimu maalum walionyesha wasiwasi na walionya juu ya madhara ambayo yangeweza kutokezea. Vikao vizito vilipangwa ili kuwapa hoja za kukubaliana na elimu mjumuisho na kuwashawishi kuwa huo ungekuwa ni mchakato unaoendelea na wenye faida za muda mrefu na kwamba walipaswa kukubali mabadiliko na kwenda na wakati. Miaka kumi baadae, bado inaelekea tumekwama njiani. Bado India inaiangalia elimu mjumuisho kuwa ni kwa ajili ya watoto wenye ulemavu tu.

Kuna kiwango kidogo cha kukubaliana miongoni mwa wataalamu wa elimu ya ulemavu. Kuna tofauti kati ya nadharia (zinazoegemea zaidi katika mtazamo wa kijamii na haki) na mtazamo uliopo sasa hivi (ambao umeegemea zaidi katika mtazamo wa kitabibu, wa uchunguzi, na tathmini. Shule ambazo zinajisifu kuwa vinara na zinatekeleza elimu mjumuisho, katika hali halisi zimeanzisha shule maalum (wanaziita vituo vya raslimali) ndani ya shule za kawaida. Baadhi ya wafuasi katika jamii ya elimu mjumuisho hawafurahii hali hii, kutokana na utata wa dhima na dhamana. Kuwepo kwa walimu wa shule za kawaida ambao wanashangaa hali hiyo pamoja na wazazi wenye wasi wasi juu ya utaratibu huo, kunazidi kuchafua hali ya mambo ilivyo.

Tukiwa ni wanachama wa jumuiya ya waelimishaji wa elimu mjumuisho, kinachotusumbua ni kwamba ingawa sera na dhamira za elimu maalum zina nia njema, katika miaka ya hivi karibuni hazijatilia mkazo sana elimu mjumuisho. Kinyume chake, zimekuwa zikianzisha na kuimarisha kuwepo kwa hali ya ubaguaji katika shule za kawaida. Miaka minne iliyopita, kulikuwa na kazi ya kusisimua kwa shirika moja lisilo la kiserikali ya kuanzisha shule ya msingi mjumuisho nchini India. Hii ilikuwa ni fursa nzuri ya kuanzisha shule mjumuisho hasa ambayo itaunganisha nadharia na vitendo. Hapa hatutaki kusimulia hadithi kuhusu uanzishwaji wa shule hiyo, lakini tutaelezea kidogo machakato wa mawazo uliofanikisha uanzishwaji wa shule hiyo.

Tulianza kwa kuchunguza mifano iliyokuwepo ya shule mjumuisho na kugundua upungufu uliokuwepo kati ya nadharia na vitendo. Pia tuligundua kuwa tulikuwa tukipingana na imani na mawazo yaliyojenga misingi ya elimu mjumuisho nchini India. Zoezi hili lilipelekea kuwa na mawazo mapya ambayo hatimaye yalionesha mfumo wetu wa mjumuisho ambao umefupishwa kama ifuatavyo:

Mawazo yaliyopo sasa Mawazo mapya
Elimu mjumuisho inahusu watoto wenye ulemavu tu. Mjumuisho hauhusiki na watoto wenye ulemavu tu. Unahusika na watoto wote, unashughulikia kuondoa ubaguaji wa aina zote kwa ajili ya kuleta elimu bora kwa wote.
Watoto wote wenye ulemavu wanahitaji elimu maalum. Si kila mtoto mwenye ulemavu anahitaji elimu maalum. Kuwa na ulemavu haimaanishi kuwa lazima utahitaji elimu maalum.
Watoto wenye ulemavu tu ndio maalum. Watoto wasio na ulemavu hawahitaji msaada au uangalizi maalum. Kila mtoto ni maalum. Mwanafunzi yeyote anaweza akapata vipingamizi katika elimu na hivyo kuhitaji msaada wa kudumu au kwa muda fulani tu.
Ni jumuia fulani tu za ulemavu zisizo za kiserikali ndizo zenye utaalamu wa sera na uendeshaji wa elimu mjumuisho Washika dau wengine nao pia wana uzoefu na utaalamu wa kutosha. Jumuia za ulemavu zisizo za kiserikali ni wanachama muhimu miongoni mwa washika dau hao katika kutunga sera na utekelezaji wa mjumuisho.
Mazingira ya shule za kawaida yalivyo sasa hivi yanafaa na ni mazuri kwa kusomea. Mazingira ya shule za kawaida yanahitaji kufanyiwa mabadiliko na kupangwa upya ili yawe mazuri kwa kusomea.
Walimu wa elimu maalum ndio wataalamu wa mjumuisho ambao wanaweza kuwaongoza walimu wa kawaida Katika elimu mjumuisho hakuna wataalamu wanaojitosheleza. Inahitaji ujuzi wa walimu wa elimu maalum na kawaida- ni njia ya katikati ambayo itaunganisha mazuri ya mfumo wa elimu maalum na mazuri ya mfumo wa elimu ya kawaida pamoja na mawazo mapya katika kuinua ubora wa elimu kwa wote.
Jukumu hasa la kutekeleza elimu mjumuisho ni la walimu wa shule za kawaida Walimu wataweza kutekeleza elimu mjumuisho iwapo kila mmoja miongoni mwa washika dau wengine atatekeleza sehemu yake ya wajibu.
Kuwafanyia uchunguzi na kuwatambua wenye na wasio na mahitaji maalum ya kielimu, kunawasaidia wenye mahitaji maalum kuweza kujumuishwa. Uchunguzi na utambuzi ukifuatiwa na mipango ya masomo kwa mwanafunzi mmoja mmoja inapelekea kuweko kwa ubaguaji na pia huyabana matarajio ya mitaala.
India inaweza kuiga kama ulivyo, mfumo wa elimu mjumuisho wa nchi za Kaskazini. Mfumo wa elimu mjumuisho, ni lazima uundwe kulingana na mazingira halisi ya India
Kwa kuwa katika baadhi ya nchi za Kaskazini elimu mjumuisho haikufanikiwa, basi pia haiwezi kufanikiwa India India ina mifano mizuri ya mambo ya kijadi ya mjumisho ambayo yanaweza pia kuigwa na nchi za kaskazini. Kutokufanikiwa kwa elimu mjumuisho katika nchi nyingine, haimaanishi kuwa elimu mjumuisho haitafanikiwa India pia.
Sera za elimu mjumuisho na sheria za nchi zinatosheleza kupelekea mabadiliko katika mfumo wa elimu. Utayari mdogo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii katika kuifanyia kazi elimu mjumuisho, usirudishe nyuma imani yetu na jitihada zetu.

Hitimisho: Mchakato wa kupitia upya mtazamo wa elimu mjumuisho ili uendane vizuri na mazingira ya India umechukua muda. Hata hivyo, hiyo iliwezekana baada ya kubadilisha mawazo na imani zilizokuwepo kuhusu elimu mjumuisho na kuanzisha mawazo ya msingi mapya kuhusu elimu mjumuisho. Ingawa hapa haukufafanuliwa, mtazamo huu mpya wa elimu mjumuisho umepelekea kuwapo kwa hazina kubwa ya mbinu mpya zenye ubunifu, mambo mengi ya kujifunza na mapendekezo ambayo yanaweza kutumika katika kuimarisha elimu katika jamii kwa ujumla. Mafanikio yetu yamezidi kuimarisha ahadi yetu ya kuifayia kazi elimu mjumuisho kwa kuwa na mitazamo yenye ubunifu, ambayo tunaweza tukaielezea zaidi na kukupatia iwapo utawasiliana nasi moja kwa moja. Mawazo mapya ya msingi tuliyoanzisha yanawezakuwa hayapendezi kwa jamii ya walimu wa elimu maalum, kwa vile utekelezaji wa mtazamo huu mpya unahitaji mageuzi makubwa ya kifikra na vitendo. Mtazamo huu mpya unaitaka jamii kupitia upya au hata kuachana na taratibu za msingi zilizopo hivi sasa. Hata hivyo, kwa wengi miongoni mwetu sisi tulio katika uwanja wa elimu maalum, tunaziona dhima hizi na mwelekeo huu mpya ni vyenye kuvutia na bora zaidi katika kuimarisha elimu kwa wote katika jamii.

Kanwal Singh amekuwa akifanya kazi katika sekta ya elimu kwa miaka 25 sasa na anaweza kupatikana kupitia: kanwalsingh.in@gmail.com. Ruchi Singh ni mtaalamu katika maswala ya Kujiendeleza Kitaalamu ambaye kwa wakati huu anatayarisha mtaala jumuishi na mazingira ya kujifunzia. Anaweza kupatikana kupitia: ruchi.singh.0511@gmail.com