This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-15/

Tathmini ya Mjumuisho katika shule za Kawaida, Ghana

Patrick Thomas Otaah, Agnes Arthur na Sandrine Bohan-Jacquot

Swali muhimu kwa ajili ya mpango wowote wa elimu mjumuisho ni: jinsi gani tutajua kama juhudi zetu zinawasaidia watoto zaidi kupata kwenda shule, na kuweza kushiriki katika mafunzo na maswala ya kijamii katika shule? Katika kujibu swali hili, Idara ya Mahitaji Maalum ya Kielimu, (Special Education Needs Division, SPED) ya Huduma za Elimu, Ghana (Ghana Education Service, GES) imeanzisha orodha itakayosaidia kuwepo na utaratibu mzuri zaidi wa ufuatiliaji wa mjumuisho wa watoto wenye ulemavu katika ngazi ya shule.

Elimu Mjumuisho Ghana 
Serikali ya Ghana imeazimia kutoa elimu ya msingi bure, lazima na bora kwa watoto wote. Mpango wa elimu mjumuisho unalenga kuongeza uandikishaji na fursa za kujifunza kwa watoto wenye ulemavu katika shule za kawaida na kujenga mazingira bora kwa watoto wa shule na mifumo ya msaada. Kwa sasa kazi kubwa ni kuelekeza nguvu katika mjumuisho wa watoto wenye ulemavu wa kiasi (less severe disabilities). Tangu 2012, SPED, kupitia kwa msaada wa UNICEF, imefanikiwa kutekeleza shughuli za elimu mjumuisho – kwa kuongeza umuhimu kwa serakali na jamii, katika uchunguzi wa watoto; mafunzo kwa walimu; na marekebisho ya vifaa – katika wilaya 12. Kumekuwa na mabadiliko ya mtazamo na sasa kuna mipango ya kueneza mtazamo huo chanya kitaifa.

‘Elimu mjumuisho ilisaidia kutatua tatizo la watoto wenye ulemavu kufanyiwa kebehi na walimu.’ Mzazi kutoka Wilaya ya Savelugu Nanton, Juni 2013.

Hata hivyo, ilikuwa ni muhimu kujifunza zaidi kuhusu athari za hatua hizi katika ngazi ya shule na darasa. Kwa vile hakukuwepo na mfumo wa ufuatiliaji kutathmini kiwango cha mjumuisho katika shule, SPED ilianzisha orodha ya kuwezesha ufuatiliaji wenye utaratibu mzuri zaidi – Kipimo cha Usimamizi wa Elimu Mjumuisho – the Inclusive Education Monitoring Tool (IEMT).

IEMT inaonesha kuwa mahitaji maalum ya watoto wenye ulemavu hayapatikani kwa njia ya marekebisho ya jumla ya shule pekee, kwa sababu baadhi ya mbinu za ujumla za mjumuisho zaweza kusahau maswala maalum ya ulemavu (angalia UNICEF State of the World’s Children, 2013 na Tahariri ukurasa wa 2-3). IEMT hukusanya takwimu zinazohusu watoto wenye ulemavu katika shule za kawaida, ili kuziba pengo kubwa la data Ghana, na kutathmini upatikanaji wake, ushiriki na mafanikio ya kitaaluma.

Kipimo cha Usimamizi wa Elimu Mjumuisho (IEMT)
IEMT inatumia viwango vya kimataifa vilivyorekebishwa, kusadifu mazingira ya ndani, na kinakusanya taarifa za kimaelezo na za kiidadi. Taarifa hizi hukusanywa na walimu wakuu, ikiwa ni pamoja na michango kutoka kwa walimu wengine wakati wa mikutano ya shule, na kisha hukaguliwa na wasimamizi, ambao kwa kawaida hutembelea na kusaidia shule mbali mbali pamoja na walimu wakuu. Wasimamizi hao hukagua vifaa vilivyopo shuleni, wakachunguza vyumba vya madarasa, na kufanya mahojiano yasiyo rasmi na walimu,watoto wenye ulemavu pamoja na wasio na ulemavu, na kisha kutoa maoni yao kwa Mwalimu mkuu na walimu wengine. Katika orodha ya Kipimo cha Tathmini ya Elimu Mjumuisho, kuna nafasi ya maoni inayoruhusu mwalimu mkuu na wasimamizi kuongeza taarifa zaidi za maswala maalum yanayohusu shule hiyo.

Kipimo hiki kinakusudia kuzisaidia shule kufanya tathmini binafsi na kutafakari kuhusu kiwango cha mjumuisho katika shule. Ufuatiliaji unafanyika mara mbili kwa mwaka (Juni na Novemba) kuangalia maendeleo yaliyopatikana na kusaidia kufanya maamuzi kwa ajili ya mwaka wa masomo unaofuata. Taarifa za ufuatiliaji huo zitatumika kama msingi kwa ajili ya tathmini inayoendelea nchini Ghana inayoangalia kiwango cha mjumuisho katika shule. Katika ngazi ya shule, taarifa hizo zitawasaidia walimu wakuu kutambua vikwazo vilivyomo ndani ya shule zao, na kushajiisha utaratibu wa kuhoji kuhusu mambo ya mjumuisho. Mfumo wa kujitathmini kwa kutaja maendeleo yaliyofikiwa (sio tu kusema ‘ ndio / hapana’) unaruhusu shule kutambua hadhi yake ya sasa na nini kinahitajika kufanywa ili kuwe na maendeleo zaidi.

Utengenezaji na upimaji wa IEMT
SPED ilitengeneza rasimu, kulingana na Vigezo vya Mjumuisho (vilivyochapishwa na Kituo cha Mafunzo ya Elimu Mjumuisho, 2007) na pia kulingana na Mwongozo wa Sera ya Elimu Mjumuisho ya Ghana (2012). Rasimu hiyo ilizingatia mazingira ya ndani; vipimo vya tathmini vilivyokuwepo, na maswala mengine yoyote ambayo hayakujitokeza katika vipimo vya ukusanyaji wa takwimu vya GES na MICS; haja ya kuwa na data za kiidadi kuhusu watoto wenye ulemavu; na umuhimu wa kuwa na kipimo cha usimamizi ambacho ni rahisi kukitumia. Mashauriano na wadau wengine katika ngazi ya kitaifa na wilaya yalifanyika, na kufanya warsha ya mwisho mwezi Juni 2013.

Baadae IEMT ilifanyiwa majaribio. Timu tano za wafanyakazi wa SPED / UNICEF na wasimamizi walioongoza tathmini hiyo katika shule 22 za kawaida za vijijini na mijini zilizochaguliwa kwa njia ya bahati na sibu iligundua kwamba IEMT ilikuwa inaeleweka kirahisi kwa watumiaji. Mabadiliko madogo yalifanywa baada ya kupima kwa kupunguza maneno au vipengele vilivyokuwa vinaleta ugumu kufahamika na kuongeza data juu ya mahudhurio ya walimu na hadhi zao (amesomea / kujitolea), na juu ya maswala ya mazingira ya ndani (kwa mfano watoto wanaohamahama). Matokeo yalionesha jinsi gani changamoto (kama vile uhaba wa walimu waliopata mafunzo, utoro wa walimu na mbinu dhaifu za ufundishaji) zinavyoathiri vibaya uwezo wa shule kuwakaribisha watoto wote, ikiwa ni pamoja na wale wenye ulemavu na mahitaji mengine maalum. Kama ilivyotarajiwa katika hatua ya majaribio, nusu ya shule zilikuwa bado hazijaanza kushughulikia elimu mjumuisho hasa, na nusu zilikuwa katika hatua za mwanzo, lakini hazikuwa na fursa kubwa ya huduma za rufaa au msaada; ingawa zilionekana kuwa na mtazamo chanya na utambuzi wa haki za elimu ndani ya shule na jamii. Majaribio hayo pia yalisaidia kutambua wadau wengine ambao walikuwa tayari wanaendelea kufanya kazi katika maswala ya elimu mjumuisho na ulemavu.

Maudhui ya IEMT

  1. Orodha ya viashiria 25 pamoja na kisanduku cha maoni
  2. Orodha ya vipengele 15 vya takwimu juu ya watoto wenye ulemavu; data zilizogawanywa kwa mujibu wa ulemavu / mahitaji
  3. Mwongozo kwa ajili ya mchakato wa ufuatiliaji (uwekaji nambari, ziara katika shule, n.k).

Vipimo vya ziada vilitengenezwa ili kuwasaidia Wakuurugenzi wa Wilaya kuelewa hali ilivyo na kusimamia rasilimali zilizopo ndani ya wilaya zao:

  1. orodha ya watoto wenye ulemavu na mahitaji mengine maalum, yenye maelezo ya kina kuhusu mahitaji na msaada pamoja na maelezo ya kina juu ya hali ya sasa ilivyo katika utoaji wa huduma kwa kila mtoto
  2. orodha ya wadau wa elimu mjumuisho na ulemavu (kwa mfano mashirika ya watu wenye ulemavu, Jumuia zisizo za Kiserikali, vituo vya rasilimali, shule maalum, wafadhili binafsi n.k)
  3. orodha ya walimu mahiri (kama wanvyoonekana na walimu wenzao) ambao wanaweza kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa kwa utendaji wao bora.

IEMT itaanza kutumika katika wilaya 12 zilizoteuliwa kuanzia mwanzoni mwa mwaka wa kitaaluma 2013/14. Matokeo yataiwezesha SPED kuimarisha mipango yake ya baadaye katika shughuli za elimu mjumuisho katika jitihada za kusaidia kupatikana kwa mahitaji ya kielimu ya watoto wote nchini Ghana.

Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana na Mr. Patrick Thomas Otaah, SPED Mkurugenzi Msaidizi otaahtp@yahoo.com,
Bibi Agnes Arthur, Afisa Elimu wa UNICEF
www.unicef.org org
Bibi Sandrine Bohani-Jacquot, Mtaalamu wa Elimu na Mjumuisho, bohan.jacquot@gmail.com 
Ofisi ya UNICEF Ghana, S.LP. AN 5051, Accra-North, Ghana

A practical science class in Choggu Primary A

Wanafunzi wakiwa katika somo la Sayansi
kwa Vitendo katika Shule ya Msingi Choggu A