This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-14/

Safari kuelekea Elimu Mjumuisho, Myanmar

Mari Koistinen na Tha Uke

Kwa miongo kadhaa Myanmar imekuwa ikitawaliwa na udikteta wa kijeshi ambapo maswala ya ulemavu hayakuonekana muhimu. Myanmar imeanza kuzingatia maswala haya kuanzia mwaka wa 2011, na sasa kuna ongezeko la shauku katika kuendeleza elimu kwa watoto wenye ulemavu. Nchi hiyo imekuwa na sera ya elimu mjumuisho tangu mwaka 2004 – iliyotokana na msukumo wa malengo ya kimataifa ya Elimu kwa Wote ambayo yanatoa wito kwa watoto wenye ulemavu kupatiwa elimu katika shule za kawaida – lakini kiwango cha utekelezaji bado hakijawekewa kumbukumbu vizuri. Hata hivyo, kumekuwa na maendeleo kadhaa yanayoendelea kufanywa. Kituo cha Eden kwa ajili ya Watoto wenye ulemavu (The Eden Centre for Disabled Children, ECDC), kwa mfano, kimekuwa kikitetea elimu mjumuisho kupitia njia ya mijadala nchini Myanmar. Katika makala hii, Tha Uke na Mari wanatoa maelezo mafupi kuhusu kazi inayofanywa na kituo cha ECDC, mafanikio yao na changamoto.

Utangulizi
ECDC ni asasi isiyokuwa ya kiserikali (NGO) kwa watoto wenye ulemavu wa viungo na akili, iliyoanzishwa Aprili 2000 na Bwana Tha Uke na Bi Lilian Gyi. Kwa miaka kadhaa sasa tokea lianzishwe, shirika hilo limeanza kukidhi mahitaji ya watumiaji wa huduma zake. Sasa lina shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na juhudi za kusaidia mapema kabla ya matatizo kuwa makubwa (early intervention), elimu maalum, ushauri nasaha, ushauri kuhusu afya ya mwili, na usahuri kuhusu masuala ya kazi, na elimu mjumuisho.

Kazi za ECDC 
Tha Uke amekuwa akiitetea elimu mjumuisho nchini Myanmar kwa miaka mingi. Kupitia msaada wa kifedha kutoka kwa Welthungerhilfe, ambayo ni Jumuiya ya kimataifa isiyo ya Kiserikali kutoka Ujerumani, ECDC iliweza kuanzisha mradi wa elimu mjumuisho mwaka wa 2007, kwa lengo la kukuza na kutetea elimu mjumuisho nchini Myanmar. Mradi huo umefanya kazi ya kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu katika shule za kawaida katika vitongoji 10 vya Divisheni ya Yangon. Kazi hiyo imelenga kutoa vifaa na mazingira yasiyo na vikwazo, na kuongeza ufahamu wa maswala ya ulemavu na mjumuisho. ECDC imefanikiwa kuandaa warsha za kuhamasisha na kupeana uzoefu kuhusiana na maswala ya elimu mjumuisho na ulemavu kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na: walimu wakuu, maafisa wa elimu, walimu kutoka shule maalum na zile za kawaida, na maafisa kutoka Idara ya Ustawi wa Jamii ambayo ndiyo inayosimamia shule maalum chache zilizopo. Warsha zimekuwa zikifanyika angalau mara moja kwa mwaka katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Mradi huo pia umeweza kusambaza vifaa vya kujifunzia, vifaa saidizi na vifaa vya kusaidia mwendo kwa watoto.

Kuongoza njia

Maung Saing Win Htay ana ulemavu wa viungo na ni mmoja kati ya walengwa wa mradi wa elimu mjumuisho. Mradi ulitoa msaada na marekebisho katika maswala ya walemavu kama vile viti vya magurdumu kwa ajili ya walemavu, kuzifanyia marekebisho njia katika mazingira ya shule, na kuweka choo cha kukalia ili kufanya usafi wa mazingira kupatikana. Mradi huo pia ulisaidia safari za Maung Saing Win Htay kwenda katika kliniki ya afya wakati anapojisikia vibaya. Aidha, mradi huo ulitaka kufanya mabadiliko katika shule na jamii nzima, kwa kuongeza ufahamu wa elimu mjumuisho miongoni mwa walimu, wanafunzi, wazazi na viongozi wa jamii. Mbinu hizi mbalimbali zilimwezesha Maung Saing Win Htay kupata nafasi ya kwenda na kubaki shule, la sivyo angekuwa yuko nyumbani tu. Sasa, Maun Saing Win Htay anakuchukuliwa kama ni wakala kwa ajili ya mabadiliko kwa watoto wengine wenye ulemavu katika jamii yake, akiwa yeye ndiye mtoto wa kwanza mwenye kutumia kiti cha magurudumu kuhudhuria shule ya kawaida. Jambo hili halionekani tena kuwa ni ajabu (mtoto anayetumia kiti cha magurudumu kwenda shule ya kawaida), na walimu wake wamejifunza mengi kuhusu ulemavu na sasa wako tayari kuwakaribisha shule watoto wengine wenye ulemavu.

Kiini cha kazi inayofuata
Moja ya changamoto kubwa zinazoikabili ECDC ni kukosekana kwa ufahamu kuhusu elimu mjumuisho miongoni mwa wadau wa elimu, ikiwa ni pamoja na watunga sera. Kuna haja ya haraka ya uhamasishaji wa kina na na utetezi katika ngazi zote. ECDC inaamini kuwa elimu mjumuisho ni lazima iwe sehemu ya mafunzo ya ualimu yaani mafunzo ya kabla na baada ya kuingia kazini ( pre- and in-service teacher training). Na pia elimu mjumuisho itoe ushauri wa vitendo kwa walimu kuhusu jinsi ya kuwafundisha watoto wenye ulemavu. Kuimarisha mkabala wa sekta mbalimbali ni muhimu, kama ilivyo muhimu kuwahusisha wadau wote katika mchakato – kujikita katika kuzingatia ushirikishwaji wa wanafamilia ni muhimu sana.

Contact:
Tha Uke, Muasisi mwenza na Mkrugenzi wa ECDC
Mari Koistinen, Mshauri Mwelekezi katika maswala ya ulemavu, Myanmar, koistinenmari@hotmail.com

Eden Centre for Disabled Children, No. (56), Wa Oo 4th Street, Phawhkan Insein Township, Yangon, Myanmar