This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-1/

Tahariri

Elimu Mjumuisho haihusu ulemavu tu na kuwaweka watoto wenye ulemavu katika shule/madarasa yenye mjumuisho. Elimu mjumuisho ni mchakato na mfumo mpana zaidi unaolenga kuimarisha sera, harakati, mitazamo/hisia, mazingira na nyenzo ili kuwezesha watoto kupata elimu bora katika katika shule iliyo karibu nao.

Kama wewe ni msomaji wa kawaida wa jarida hili na tovuti ya EENET, basi utayaelewa mawazo haya. Ujumuishaji wa watoto wenye ulemavu, unabakia kuwa ni swala muhimu sana katika elimu mjumuisho, ingawaje elimu mjumuisho haihusiani na ulemavu tu.

Kwa miaka mingi sasa kumekuwa na mawazo kwamba Kampeni ya Elimu Duniani na mbinu kama vile shule rafiki kwa mtoto, havijaweza kwa ukamilifu kuzingatia mahitaji ya vifaa na ushirikishwaji kwa wanafunzi wenye ulemavu. Mbinu za ujumla za mjumuisho hazijaweza bado kuleta mafanikio makubwa kwa watoto wenye ulemavu, ingawa zimeleta matokeo yanayoonekana wazi katika kuimarisha ubora wa elimu, ufundishaji, mitazamo n.k. Baadhi ya vipingamizi kwa watoto, haviwezi kuondolewa kwa kuimarisha elimu ya kawaida tu.1 Wakati mwingine mipango ya elimu mjumuisho imekuwa ikisitasita katika kushughulikia mambo maalum yanayohusu ulemavu peke yake.

Swala hili limekuwa likiwatanza watekelezaji na watungaji wa mipango na sera za elimu. Wakichukua upande mmoja tu kuna hatari ya kuegemea zaidi katika kushughulikia mahitaji maalum ya ulemavu na kuonekana kuwa hawana mtazamo wa kina zaidi unaohusu mjumuisho kwa ujumla pamoja na mabadiliko ya shule kwa ujumla.

Hata hivyo, si lazima kwa programu na sera kuelekezwa katika upande mmoja wapo kati ya hizo mbili. Bali inawezekana kabisa (na ndivyo inavyotakiwa hasa) kwa programu au sera za mjumuisho kuchukua mwelekeo wa pande zote mbili yaani kushughulikia kuimarisha mfumo mzima wa elimu na mazingira ya shule na wakati huo huo kushughulikia mahitaji maalum kwa mwanafunzi mmoja mmoja na hasa wale wenye ulemavu. Kushughulikia mahitaji maalum ya watoto wenye ulemavu ni kipengele muhimu katika mbinu za ufundishaji zinazomlenga mtoto ambazo ni mbinu muhimu sana katika kukuza ubora wa elimu kwa ujumla.

Wazo hili la Ufuatiliaji Sambamba si geni, bali limekuwa likisahaulika. Kutokana na hali hiyo tumeona ni wakati mwafaka sasa kuwa na toleo maalum katika jarida letu kuamsha fikra kuhusu namna haki na mahitaji ya ulemavu yanavyoweza kushughulikiwa katika mfumo wa elimu mjumuisho kwa kutumia mwelekeo wa Ufuatiliaji Sambamba.

Huu umekuwa ni wakati mwafaka zaidi kwa vile wazo kuu la Kampeni ya Elimu Duniani, 2014 limejikita katika Ulemavu na Elimu Mjumuisho. Kampeni hii ambayo huifikia hadhira kubwa ulimwenguni wakiwemo watunga sera na watekelezaji, huchukua pia mwelekeo wa upatikanaji wa haki katika maswala ya elimu. Kwa hivyo, kampeni hii itatoa wito kwa elimu mjumuisho kuwa ni kiungo muhimu cha kupelekea kupatikana kwa haki ya elimu kwa watoto wote wakiwemo wale wenye ulemavu. Kampeni hii pia inatambua umuhimu wa mwelekeo wa “ufuatiliaji sambamba”; kwa kutoa mapendekezo kwa serikali za mataifa mbali mbali pamoja na jamii ya kimataifa kwa ujumla kuchukua hatua zitakazosaidia kuleta mabadiliko ya mifumo na harakati za kusaidia wanafunzi wenye ulemavu.

Makala katika jarida hili yanatoa mitazamo na mifano mbali mbali kuhusu kuwajumuisha watoto wenye ulemavu. Sisi kama wahariri, hatutatoa maamuzi iwapo waandishi wametumia mtazamo wa “ufuatiliaji sambamba” au la, bali tunakuachia wewe msomaji utafakari na pengine kutoa maoni yako na uzoefu wako kupitia katika ukurasa wetu wa facebook.2 Iwapo ungependa kufahamu zaidi kuhusu mtazamo wa “ufuatiliaji sambamba”, angalia Rieser (2013) – Maelezo katika Tanbihi 1. Makala kutoka Kambodia pia yanatoa maelezo yaliyo rahisi kuhusu mtazamo wa “ufuatiliaji sambamba”

Kuelewa mtazamo wa ufuatiliaji sambamba kunaweza kuwachanganya watunga sera na watendaji. Makala kutoka Kameruni, India na Malaysia yanatoa tafakuri binafsi juu ya safari ya watendaji hao katika kuelekea kuielewa na kuitekeleza elimu mjumuisho. Makala kutoka India hususan, inaonesha mageuzi ya mtazamo wa fikra za kuzingatia zaidi mahitaji maalum ya ulemavu hadi katika mtazamo wa elimu mjumuisho. Wazo kuu la Kampeni ya Elimu Duniani lilikuwa ni Walimu na Elimu ya Ualimu. Kurasa za katikati ya toleo hili (pamoja na kipeperushi kilichomo ndani) zinatoa mikakati mitano ya kuhakikisha kwamba walimu wanaweza kutoa elimu bora na msaada kwa wanafunzi wenye ulemavu. Makala kutoka Bulgaria pia inaonesha mchakato wa kufikiria tena kuhusu namna walimu wanavyofunzwa kuhusu mjumuisho na ulemavu.

Katika mtazamo wa ufuatiliaji sambamba katika elimu mjumuisho,utoaji wa msaada unaolengwa kwa watoto wenye ulemavu, mara nyingi hutolewa na walimu wa muda – kama vile ilivyofafanuliwa katika makala kutoka Togo na Cambodia – ambao hufanya kazi moja kwa moja na watoto wenye mahitaji maalum pamoja na walimu wa kawaida. Vile vile, vituo vya asasi na timu zinazoundwa na watu wenye taaluma mbali mbali zinaweza kusaidia mabadiliko ya shule nzima na kushughulikia mahitaji ya watoto ya ushiriki na ya kujifunza kama inavyooneshwa katika Makala ya China na Kambodia.

Mchango muhimu ambao watu wenye ulemavu wanaweza kutoa katika elimu mjumuisho, unafafanuliwa katika makala kutoka Iraki na Papua New Guinea. Nchini Iraki, mitazamo ya watu kuhusu ulemavu imeingizwa katika mafunzo ya ualimu na katika nchi ya Papua New Guinea, viziwi wamepewa mafunzo ya kuwa walimu wasaidizi wakisaidia ujumuishaji wa wanafunzi viziwi.

Jambo la kushangaza ni kwamba, katika makala za mwaka huu, sauti za watoto hazikupewa nafasi. Kwa hivyo, tunawahamasisha wasomaji wetu kutafakari juu ya umuhimu wa kusikiliza maoni ya watoto kuhusu elimu mjumuisho na kushirikiana nasi (na pia mtandao wa kimataifa) juu ya uzoefu wako wa kuwawezesha watoto kusema kuhusu kujumuishwa / kutengwa, kubaguliwa na utofauti, ulemavu, haki, n.k.

 

1 Kwa mtazamo wa kina kuhusu maswala haya angalia: Rieser, R (2013) ‘Teacher Education for Children with Disabilities. Literature Review’. Prepared for UNICEF, New York. http://bit.ly/18AGOAi
2Ukurasa wa facebook wa EENET: http://on.fb.me/1gIbwtW

Katika kuelekea kwenye Kampeni ya Elimu Duniani, 2014, (Wiki ya Kimataifa ya Vitendo ni Mei). Tunakukumbusha kushirikiana na Muungano wa GCE katika nchi yako. Tumia fursa hii ya Kampeni ya Elimu Duniani kuongeza na kuimarisha juhudi za utetezi na ushawishi katika kuonesha harakati zako kuhusu elimu mjumuisho. Vile vile, hamasisha watendaji wa shule za kawaida katika kuimarisha elimu mjumuisho na kufikiri kuhusu maswala ya ulemavu. Hebu na tuunde kampeni iliyo imara!

Habari muhimu:

Toleo hili limechapishwa kwa pamoja kati ya EENET na IDDC, mtandao wa kimataifa wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kuhusu ulemavu na mjumuisho. Kikosi Kazi cha Elimu Mjumuisho cha IDDC kinafanya kazi mbali mbali za utetezi wa elimu mjumuisho na kutoa mwongozo kwa watendaji na watunga sera. Pia kinashiriki kikamilifu katika kutoa habari na kuikuza Kampeni ya Elimu Duniani. Unaweza kuwasiliana na IDDC katika:

rue Washington 40, B-1050 Brussels, Belgium
info@iddcconsortium.net
www.iddcconsortium.net

Tunawashukuru sana wafuatao, ambao wengi wao ni wanachama wa IDDC, kwa kusaidia kifedha uchapishaji wa toleo hili:

Atlas Alliance
CBM logo
Handicap International logo
Light for the World
NAD
NFU
NORAD
Save the Children