This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-11/

Uanzishaji wa vituo vya raslimali kwa ajili ya Elimu Mjumuisho, China

Ming Liu

Moja ya changamoto muhimu katika kuendeleza elimu mjumuisho ni kwamba shule za kawaida zinahitaji mafunzo ya mara kwa mara yanayoendelea na sio mafunzo ya kozi zinazotolewa mara moja tu. Zinahitaji mafunzo hayo ili ziwasaidie wafanyakazi na wadau wengine kudumisha motisha huku wakiendeleza ujuzi na kujiamini kuwa wabunifu zaidi na katika kutekeleza mjumuisho zaidi. Msaada wa utekelezaji wa elimu mjumuisho unaweza kutolewa katika njia tofauti. Katika makala hii, Ming Liu anaelezea jinsi vituo vya nyenzo kwa ajili ya elimu mjumuisho vinavyoanzishwa nchini China, kama njia ya kuunga mkono sera na mabadiliko katika ngazi za chini.

Utangulizi
Nchini China, Shirika la Hifadhi ya Watoto (Save the Children) linafanya kazi na wilaya saba katika Mkoa wa Sichuan, Mkoa wa Yunnan na Xinjiang Uigur Mkoa wenye Mamlaka yake kuanzisha mfumo wa elimu mjumuisho na kuimarisha huduma kwa watoto wenye ulemavu. Mradi huu wa miaka mitatu ulianza mwezi Julai 2012 na unalenga kuanzisha vituo vya raslimali, na kufanya kazi katika shule za kawaida zilizochaguliwa kwa ajili ya majaribio, kutoa mafunzo kwa walimu wakuu na walimu wengine, na pia kutoa mafunzo kwa walimu wa shule za elimu maalum, ili kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu mchanganyiko na wenye ulemavu mkubwa. Vituo hivyo vitasaidia mfumo wa elimu mjumuisho na vitahakikisha kuwa huduma zitaendelea hata baada ya mradi kukamilika. Mradi bado ni mpya sana, hivyo makala hii inalenga kubadilishana uzoefu wetu katika hatua ya awali ya uanzishaji wa mradi huo. Tunatumai kuwa na uwezo wa kutoa taarifa za maendeleo ya mradi huo katika toleo la baadaye la jarida hili.

Majukumu ya Vituo
Vituo hivyo husimamiwa na taasisi za elimu katika ngazi ya mkoa, na vinatarajiwa kuchukua majukumu mengine kadhaa, ikiwa ni pamoja na: uongozi wa elimu; mafunzo ya ualimu, na kufundisha utafiti kwa walimu; kuratibu baina ya idara moja na nyengine, uratibu; utoaji wa huduma za matengenezo, ushauri, vifaa saidizi na vifaa vyengine.

Kuhusu wanafunzi wenye ulemavu, vituo hivi vina jukumu la:

  • kuanzisha sera katika ngazi ya jimbo kuhusu elimu ya watoto wenye ulemavu kulingana na sera ya elimu ya mkoa
  • kutunga taratibu na kanuni zinazohusiana na: uchunguzi na utambuzi wa watoto wenye ulemavu ambao watahitaji msaada wa mtaalamu katika elimu; uandaaji na utekelezaji wa mpango wa elimu wa mtu binafsi (IEP); tathmini ya shule /utendaji wa walimu katika kukidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu, n.k
  • kufuatilia shule za kawaida kwa lengo la kutoa msaada uliokusudiwa na vile vile kwa ajili ya tathmini ya maendeleo ya elimu mjumuisho.
  • kuratibu pamoja na serikali ya jimbo, ‘ Shirikisho la Watu wenye Ulemavu na, Ofisi ya Huduma za Wananchi juu ya kazi ya kutafuta watoto wenye ulemavu, kukusanya na kubadilishana taarifa, na kuimarisha huduma za rufaa.
  • Kutoa mafunzo kwa walimu wa kawaida na walimu walio katika vituo kutoka shule za kawaida ili wawe na uwezo mkubwa zaidi wa kuwasaidia watoto wenye ulemavu
  • kutengeneza vifaa saidizi vya kufundishia na kujifunzia.
  • kutoa huduma za ukarabati kwa ajili ya watoto wenye umri wa shule wenye ulemavu, ama katika vituo au kwa njia ya huduma kwa jamii
  • kutoa ushauri kwa wazazi, na kuandaa mafunzo kwa wazazi na kuandaa shughuli mbali mbali za uhamasishaji.

Kuhakikisha uendelevu 
Kuanzisha kituo cha raslimali kama hiki ina maana kuwa kutakuwepo na mabadiliko katika mfumo wa utawala wa elimu. Inategemea ujasiri na nia ya Mamlaka ya Elimu katika jimbo kuleta uvumbuzi katika usimamizi wa elimu, kufafanua upya majukumu ya kila idara, kupanga upya rasilimaliwatu na bajeti, na kuanzisha sera na kanuni mbali mbali za kuendesha elimu mjumuisho. Kwa hivyo basi, shirika la Hifadhi ya Watoto (Save the Children) lilihitaji washirika madhubuti ili kusaidia mpango huo kwenda mbele, na kuwa endelevu kwa muda mrefu.

Kwa hivyo, Majimbo yalialikwa katika jitihada za kutafuta washirika katika mpango huu, kufuatia mkutano wa ufunguzi wa mradi. Uteuzi wa majimbo ulifanywa na shirika la Save the Children pamoja na idara za elimu za mikoa kulingana na orodha ya vigezo muhimu. Mchakato huu ulipelekea Majimbo saba kuchaguliwa na kutia saini mikataba ya ushirikiano na Shirika la Save the Children. Kupitia ushirikiano huo, Shirika la Save the Children litatoa msaada wa kiufundi kwa ajili ya kuanzisha vituo vya raslimali, na mafunzo kwa ajili ya wafanyakazi wa taasisi ya elimu na walimu walio katika vituo hivyo.

Shirika hilo pia litatoa fedha za kuanzisha mradi huo. Kila jimbo, hata hivyo, litawajibika kutoa eneo, kupanga na kulipa wafanyakazi, kutenga bajeti ya kufanyia kazi katika vituo na kisha kukiendesha kituo hicho.

Uanzishaji wa vituo 
Vituo vya raslimali ni dhana mpya katika majimbo saba yaliyochaguliwa. Kwa hivyo, katika mkutano wa kukaribishana katika mradi, tuliwachukua wakuu wa Ofisi ya Elimu pamoja na wafanyakazi wenye dhamana katika maswala ya elimu ya msingi kwenda kutembelea vituo vinavyoendeshwa kwa ufanisi katika mji wa Beijing. Hapa wanaweza kujadiliana na maafisa elimu wa wilaya, wakuu wa vituo na wafanyakazi wengine. Ziara hii ilijenga ufahamu wa majukumu, muundo, utumishi, nyenzo/vifaa na uendeshaji wa vituo hivyo. Tuliandaa vigezo kwa ajili ya kuchagua wafanyakazi wa vituo vya rasilimali, kwa kushirikiana na Ofisi ya Elimu ya Jimbo. Kupitia msaada wa kiufundi kutoka Shule ya Wasioona ya Perkins, tuliunda timu ya wakufunzi – yenye wataalam wa elimu maalum kutoka Marekani, India na China – kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kituo cha rasilimali kupitia warsha tano kubwa, kila moja ikifuatiwa na ufuatiliaji wa moja kwa moja. Katika warsha ya kwanza, wafanyakazi kutoka kila jimbo walifanya kazi pamoja kuandaa rasimu ya mpango wao wa kituo cha rasilimali, ikiwa ni pamoja na kuangalia nafasi ya eneo la kituo, muundo wa uongozi, Utumishi, ufafanuzi wa majukumu, na rasilimali zinazohitajika. Wafanyakazi waliwasilisha rasimu za mipango yao kwa ofisi ya elimu nayo Ofisi ya Elimu itazipitia na kuziweka vizuri zaidi rasimu hizo kulingana na mazingira ya majimbo yenyewe. Hapa ndipo tulipo kwa sasa.

Fedha za kuanzishia mradi kwa ajili ya vituo zitatolewa baada ya mipango yao kuidhinishwa. Fedha hizo zitatumika kununulia vifaa vya ofisi, vifaa vya kufanyia matengenezo na vifaa vya mapambo, vitabu na vitu vya kuchezea kwa ajili ya watoto. Katika mchakato wa kuanzisha vituo hivyo, Shirika la Save the Children litafanyakazi na wataalamu wenye uzoefu na viongozi wa vituo ili kutoa ushauri kwa kila Jimbo kwa njia ya mawasiliano ya mbali na ziara katika maeneo watakayofanyia kazi. Warsha za walimu wa kituo cha rasilimali na ziara za ufuatiliaji zitafanyika ili kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanapata stadi muhimu zilizokusudiwa.

Changamoto za usoni 
Kuanzisha kituo cha rasilimali katika hali ya kukijenga itakuwa sehemu rahisi ya mradi huu. Utumishi, kupata bajeti kutoka serikali ya Jimbo, na kukiendesha kituo kwa muda mrefu itakuwa muhimu kwa mafanikio ya mradi huo. Ofisi ya elimu itabidi iishawishi serikali ya Jimbo kuwekeza katika elimu mjumuisho. Katika kubuni nafasi za kazi katika kituo cha rasilimali, kuajiri wafanyakazi na kuwalipa kutoka bajeti ya serikali, Ofisi ya Elimu ya Jimbo itahitaji kujadiliana na idara mbalimbali za serikali. Hivi sasa, wafanyakazi wa vituo vya rasilimali tuliowapatia mafunzo wanatoka katika sekta mbalimbali,zikiwemo Ofisi ya Elimu ya Mkoa, vituo vya mafunzo ya walimu katika majimbo, huduma za elimu maalum katika majimbo, na shule za kawaida. Hatimaye, tunatarajia nao watakuwa wafanyakazi wa kudumu katika vituo.

Ming Liu, Meneja wa Mradi wa Elimu Mjumuisho
Save the Children China Programme
2-2-52, Jianwai Diplomatic Compound
Chaoyang District, Beijing, PRC
ming.liu@savethechildren.org
www.savethechildren.org.cn