This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-9/

Wasaidizi wa kufunza viziwi: utoaji wa fursa za elimu na ajira kwa watoto na watu wazima viziwi nchini Papua New Guinea

Light for the World Austria

Kwa watoto wengi wenye ulemavu, ukosefu ya watu wazima wenye ulemavu katika shule za kawaida inaweza kuwa ni kikwazo kwa ushirikishwaji wao. Watu wazima wenye ulemavu wanaweza kuwa ni mfano wa kuigwa na wanaweza pia kuwafanya watoto wenye ulemavu kujiamini katika utambulisho wao. Makala hii inaelezea kuhusu utaratibu wa kuwafunza wasaidizi wa kufundisha viziwi waweze kusaidia katika ufundishaji wa watoto hao katika shule za kawaida nchini Papua New Guinea kama njia ya kuongeza elimu na fursa za ajira kwa watu wazima viziwi.

Mradi unaoendeshwa na Callan Services, unalenga kuongeza ubora wa elimu ya msingi na huduma za afya ya msingi kwa watoto viziwi. Moja ya mambo muhimu katika mradi huu, ni kuajiriwa kwa wasaidizi 20 ambao ni viziwi kabisa au wenye usikivu hafifu, ambao huitwa Wasaidizi Wafunza Viziwi.

Jukumu la wasaidizi hao ni sehemu ya juhudi kubwa za kujenga utambulisho na kukuza utamaduni wa viziwi, na kusaidia watoto 300 viziwi kwenda shule za msingi. Mradi huu pia unataka kuwapa wasaidizi hao fursa ya kupata sifa za kitaaluma (ili hatimaye wawe walimu) na kupewa mafunzo ya ukuaji wa watoto. Baadhi ya wasaidizi hao tayari wamefanikiwa kupata kiwango cha kuweza kuendelea na elimu ya juu. Wasaidizi hawa wanatambuliwa katika jamii.Wao huchaguliwa kutokana na ujuzi wao katika mawasiliano na mazungumzo kwa wote; viziwi na wasio viziwi katika jamii, na kwa uwezo wao wa kushirikiana na kufanya kazi pamoja na watoto wadogo viziwi. Wao pia huchaguliwa kutokana na ubunifu wao, na wengi wao wamefikia kiwango cha elimu ya msingi.

Wasaidizi wa kufunza viziwi hupokea mafunzo wakiwa kazini kutoka kwa mwalimu mtaalamu kutoka Deaf Education Resource Unit (DERU) (Kitengo cha Elimu ya Uziwi) (madarasa tofauti yaliyo katika shule za kawaida kinachoshughulikiwa na mwalimu wa viziwi aliyehitimu mafunzo ya elimu hiyo). Pia wanapata fursa nyingine za elimu na msaada wa kuinua kiwango chao cha Kiingereza. Wasaidizi hawa pia wana fursa ya kukutana katika mikutano katika ngazi za mkoa na taifa. Nafasi hii ya kubadilishana uzoefu ni sehemu muhimu ya kujenga na kuimarisha jamii ya viziwi. Wasaidizi pia wana majukumu mapana zaidi ya wajibu wa kusaidia darasani. Wanashiriki na kusaidia katika mitaa, mikoa na taifa, kwenye mipango ya michezo, na kusaidia katika mafundisho ya lugha ya alama.
Kwa njia ya kutoa mafunzo juu ya elimu ya utoto, mradi huu unataka kuwasadia wasaidizi hao kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na watoto wadogo viziwi na kusaidia mpito wao kutoka madarasa ya DERU kwenda katika madarasa ya kawaida. Mafunzo pia huwasaidia kuwa na ujuzi wa kusaidia marekebisho ya mtaala kulingana na mahitaji binafsi ya kila mtoto kiziwi, na wao kuwa na rasilimali katika madarasa ya kawaida.
Elimu ya viziwi ni mpya kiasi Papua New Guinea na watu wazima wengi viziwi hawajawahi kuwa na fursa ya kuona uwezo wao kama wachangiaji muhimu katika elimu wala kutambua uwezo wao wa kupata elimu ya juu na ajira bora zaidi. Mbinu ya Wasaidizi wa Kufunza Viziwi husaidia kutoa fursa za elimu pamoja na ajira. Wasaidizi hao wanakuwa ni mifano mizuri kwa watoto viziwi na familia zao katika jamii. Zaidi ya hayo, wamechangia katika kuimarisha ujuzi wa lugha ya alama mashuleni, miongoni mwa watoto na walimu.

Aidha, mradi huo, umewezesha kuanzishwa kwa Walimu wa Taifa wa Lugha ya Alama ambao wataongoza ufundishaji wa lugha hiyo. Matokeo muhimu ya mradi huo ni uamuzi wa kuendeleza zaidi Lugha ya Alama nchini Papua New Guinea, na utambuzi wa haja ya kuwa na mafunzo rasmi ya ukalimani na mafunzo kwa ajili ya kupitia kikamilifu, mitazamo ya elimu. Uendelezaji wa Lugha ya Alama nchini Papua New Guinea unaendelea kwa kuendesha warsha nchini kote, na Wasaidizi wa Kufunza Viziwi ni jambo muhimu katika mchakato huu.

Wasiliana na: Light for the World Austria

Sabine Rehbichler
s.rehbichler@light-for-the-world.org

Callan Services, Michael Lulu
Micheal.lulu@gmail.com